Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewaachia huru wachezaji Deus Kaseke na Obrey Chirwa baada ya kutowakuta na hatia katika mashtaka yaliyokuwa yanawakabili huku mwenzao Simon Msuva akitarajiwa kupewa onyo kali kwa njia ya maandishi baada ya kukutwa na hatia.
Awali kamati hiyo iliwaita wachezaji hao wawili kwa ajili ya kutoa maelezo juu ya tukio la kumuangusha mwamuzi ambalo lilikuwa linawakabili huku Msuva akikosekana kutokana na kutokuwepo nchini kwa sasa.
Kaseke na Chirwa walitiwa hatiani baada ya tukio la kumsukuma mwamuzi kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu msimu uliopita dhidi ya Mbao FC kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo Yanga walifungwa bao 1-0.
Katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Shirikisho hilo jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Ndugu Peter Hella ametangaza rasmi kuwa wachezaji hao wanaachiwa huru kutokana na kuridhishwa na utetezi wao sambamba na uthibitisho wa njia ya picha mnato, video na ripoti ya mwamuzi.
Msuva hatiani
Msuva amekutwa na hatia baada ya vielelezo vyote kuthibitisha kuwa mchezaji huyo alimwangusha mwamuzi wakati wakizozana baada ya Yanga kukataliwa goli dakika ya 85 ya mchezo huku Kaseke na Chirwa wakiachiwa huru.
Hata hivyo kamati hiyo imeshindwa kumuadhibu Msuva kutokana na kwamba kamati ya ligi ilishawasimamisha wachezaji hawa watatu kucheza mashindano yoyote ya ndani na baada ya ligi, Yanga walikuwa na mashindano ya SportPesa Super Cup na wakati huo bado Msuva alikuwa mchezaji wa Yanga, kwa maana hiyo kamati ya Ligi ilitoa adhabu kabla kamati ya nidhamu haijakaa.
Kanuni ya 49 inaitaka kamati hiyo kutoa adhabu kwa mchezaji ambayo ni kufungiwa kucheza si chini ya mechi tatu na onyo kali hivyo kwa kuzingatia kuwa Msuva alikuwa ameshatumikia adhabu kabla kamati ya nidhamu haijakaa, kamati hiyo licha ya kumkuta na hatia lakini italazimika kumtumia onyo kali kwa njia ya maandishi kulingana na ibara ya 14 baada ya kuwa ameshatumikia adhabu
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti huyo alimalizia kwa kulishauri Shirikisho la Soka nchini kuzihusisha kamati husika katika kutatua matatizo. Hiyo ni kutokana na wachezaji Deus Kaseke na Obrey Chirwa ambao hawakukutwa na hatia kuwa wameshatumikia adhabu kwa kosa ambalo limethibitika kuwa hawakulifanya, hali iliyopelekea kamati hiyo ya nidhamu kuwaachia huru licha ya kukosa michezo ya kwanza ya Ligi Kuu.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni