0

Klabu ya Real Madrid imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Spain Super Cup uliopigwa kwenye dimba la Camp Nou ambao ni uwanja wa nyumbani wa Barcelona.
Iliwabidi Real Madrid kusubiri hadi kipindi cha pili ili waweze kuondoka na ushindi huo dhidi ya vijana wa kocha Ernesto Valverde baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya kutofungana huku golikipa wa Real, Kaylor Navas akifanya kazi ya ziada kupangua mashuti ya Messi na Luis Suarez huku Ter Stegen kwa upande wake nae akifanya kazi kubwa kumzuia Gareth Bale asiweze kufunga kwa upande wa Real.
Real Madrid walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 50 ya mchezo baada ya mlinzi wa Barcelona Gerald Pique kujifunga katika harakati za kuokoa krosi iliyochongwa na Marcelo.


Andres Iniesta akipambana vikali na Toni Kroos kwenye mchezo wa Spain Super Cup ambapo REal waliondoka na ushindi wa mabao 3-1. Picha/ Barcelona-Twitter

Barcelona walisawazisha bao hilo dakika ya 77 kupitia kwa Lionel Messi kwa mkwaju wa penati baada ya golikia wa Real, Kaylor Navas kumuangusha Luis Suarez ndani ya eneo la hatari.
Hata hivyo bao hilo halikuweza kudumu kwani dakika tatu baadae, Cristiano Ronaldo aliyeingia kuchukua nafasi ya Karim Benzema aliongeza bao la pili kwa upande wa Real Madrid baada ya kuachia mkwaju mkali nje ya boksi uliomshinda Ter Stegen na kutinga wavuni kisha akazawadiwa kadi ya njano papo hapo baada ya kuvua jezi  wakati akishangilia goli hilo
Dakika mbili baadae, mwamuzi Ricardo De Burgos Bengoetxea alimzawadia kadi ya pili ya njano Cristiano Ronaldo na kumuongezea kadi nyekundu papo hapo baada ya kujiungusha ndani ya penati boksi akidai kufanyiwa faulo na mlinzi wa Barcelona Samuel Umtiti hali ambayo ilizua tafrani na kupelekea Ronaldo kumsukuma mwamuzi kwa nyuma.
Zikiwa zimesalia dakika chache mpira kumalizika, Marc Asensio aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Mateo Kovacic aliifungia Real Madrid bao la tatu kwa shuti kali nje ya penati boksi na kufanya matokeo kuwa 3-1 hadi mwisho wa mchezo.
Kwa matokeo hayo sasa, Real Madrid wanajiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa kombe la Spain Super Cup huku wakisubiria mchezo wa pili wa marudiano utakaopigwa Santiago Bernabeu Agosti 17.


Chapisha Maoni

 
Top