Manchester imeianza Ligi Kuu nchini Uingereza kwa kishindo cha aina yake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya West Ham kwenye dimba la Old Trafford jioni ya leo huku Mshambuliaji mpya wa klabu hiyo, Romelu Lukaku akifunga magoli mawili
Lukaku aliipatia United goli la kwanza dakika ya 33 ya mchezo kufutia pasi ya Marcus Rashford na hadi mpira unakwenda mapumziko United walikuwa mbele kwa bao hilo moja
Alikuwa ni Lukaku tena aliyewainua mashabiki wa United vitini baada ya kupachika bao la pili dakika ya 52 kipindi cha pili akimalizia vyema pasi ya Henrikh Mkhitaryan.
Romelu Lukaku akishangilia baada ya kuiandikia United bao kwenye mchezo dhidi ya West Ham United leo. Picha/ Manchester United-Twitter
Anthony Martial aliipatia United bao la tatu dakika ya 87 kupitia pasi ya Henrikh Mkhitaryan tena kabla ya Paul Pogba kuitimisha karamu ya mabao kwa kufunga goli la nne dakika za majeruhi baada ya kumegewa pande murua na Anthony Martial.
Kwa matokeo hayo sasa United inapanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza maarufu kama EPL ambapo kila timu imeshacheza mchezo mmoja mpaka sasa baada ya pazia la Ligi hiyo maarufu duniani kufunguliwa rasmi hapo siku ya Ijumaa.
Chapisha Maoni