0
Msimbazi klabu ya Simba, imeonyesha inautaka kweli ubingwa wa ligi kuu baada ya kuendeleza ubabe na kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-0, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Nahodha wa timu hiyo, John Bocco 'Adebayor' ndiyo alifungua kalamu hiyo ya mabao dakika ya 22 akifunga kwa kichwa pamoja na la tatu dakika ya 74 baada ta kupiga mpira mrefu nje ya 18 ukaenda moja kwa moja langoni, wakati Mdhamiru Yassin alifunga la pili dakika ya 66 akiunganisha krosi ya Shiza Kichuya.
Simba ilipata ushindi huo huku nyota wake, Emmanuel Okwi akipata majeraha dakika ya 45 na kushindwa kuendelea kipindi cha pili kutokana na kupigwa kiwiko na Mau Bofu ambaye pia alitolewa kwa kadi nyekundu.
Katika mchezo huo vilabu vyote vilionekana kushambuliana kwa kushtukiza, lakini hata hivyo viungo wa Simba walikuwa wameimarika na kupiga pasi za uhakika zilizozaa mabao.
Washambuliaji wa Shooting, Abdulrahman Mussa na Issa Kanduru, walishindwa kupenya katika safu ya ulinzi ya Simba, hata walipofanya mabadiliko kwa kumtoa Kanduru na kumuingiza Jamal Masoud bado walionekana kuteteleka licha ya kutengeneza nafasi nyingi.

Chapisha Maoni

 
Top