0
TIMU ya Azam FC imeanza vyema Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Azam FC iongoze Ligi Kuu sasa baada ya mechi za raundi ya kwanza, kutokana na kupata ushindi mzuri dhidi ya timu nyingine zilioanza vizuri msimu mpya.
Mabao ya Azam FC leo yamefungwa Joseph Mahundi dakika ya 33 akimalizia pasi ya kichwa ya Danny Lyanga aliyefunga bao la pili dakika ya 45 na ushei kwa pasi ya kiungo Mudathir Yahya.
Kipindi cha pili Mbeya City walijiimarisha na kuwazuia Azam FC kupata mabao zaidi, huku nao pia wakishindwa kupata japo bao moja.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Yanga SC imeifunga 2-1 Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stand United imeichapa 1-0 African Lyon Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati, KMC imelazimisha sare ya 0-0 na JKT Tanzania Uwanja wa Meja Isamuhuyo, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Na jana mabingwa watetezi Simba SC wealishinda 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Taifa, Ndanda FC washinda ugenini 1-0 dhidi ya wenyeji, Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Singida United walifungwa 1-0 nyumbani Uwanja wa Namfua na Biashara United na Alliance FC pia walifungwa 1-0 na wapinzani wao wa jiji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Kagera Sugar iIianza vizuri pia kwa ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Coastal Union, timu kipenzi cha Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ililazimishwa sare ya 1-1 Lipuli FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Chapisha Maoni

 
Top