Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa amesema hakuna mtu yeyote mwenye hatimiliki ya Tanzania hivyo Watanzania wote wanao wajibu wa kuilinda na kudumisha amani na utulivu uliopo.
Akitoa salamu wakati wa ibada ya kumweka wakfu Mchungaji Solomon Massangwa kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha jana, Lowassa alisema amani na utulivu ukikosekana, watu wote watadhurika bila kujali tofauti zao kidini
wala kiitikadi.
“Nchi hii ni yetu sote, hakuna mwenye hatimiliki ya nchi, kwa hiyo kanisa mna kazi kubwa ya kusaidia kuilinda amani hii tuliyonayo,” alisema Lowassa ambaye anatajwa kuwania urais wa
Tanzania.
Alisema: “Hii amani ni kama ilivyo Oxygen kwa binadamu, mtu akiikosa tu anakufa na Taifa likiikosa amani linasambaratika,” alisema.
Katika ibada hiyo iliyofanyika Usharika wa Kimandolu jijini Arusha na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikali na vyama vya siasa,
Lowassa aliwataka viongozi wa dini na
madhehebu yote kuhubiri na kuombea amani.
Pamoja na maaskofu wote wa KKKT na
madhehebu mengine, hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ambaye pia anatajwa kuwania urais na Lazaro Nyalandu ambaye amekwishatangaza nia yake hiyo lakini
wote hawakupata fursa ya kutoa salamu.
Mkuu wa KKKT nchini, Askofu Dk Alex Malasusa aliwataka wote wanaopata fursa ya uongozi serikalini kusimamia falsafa na misingi itakayohakikisha Serikali haifungamani na dini au
madhehebu yoyote katika utendaji na utekelezaji wa wajibu na majukumu yake.
“Misingi tuliyojijengea ni ya Serikali kutoongozwa kwa kufuata misingi ya dini yoyote, inapaswa kusimamiwa na kuendelezwa na wote wanaopata
fursa ya kuongoza nchi, dini isitumike
kufarakanisha Taifa, ” alionya Dk Malasusa.
Alisema kanisa linaendelea kumwombea Rais Jakaya Kikwete aendelee kuongoza kwa haki na hekima ili atakapokabidhi kijiti cha uongozi baada ya uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu, akabidhi
Taifa lenye amani na utulivu.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mary Nagu aliyemwakilisha Rais Kikwete, alitumia
jukwaa hilo kuwaomba viongozi wa dini
kusaidiana na Serikali kukabiliana na vitendo vya uhalifu yakiwamo matukio ya kigaidi.
“Dini isaidiane na Serikali kwa kuwafundisha waumini utii wa sheria, Katiba na taratibu za nchi
ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu kama matukio ya milipuko ya mabomu na watu kumwagiwa tindikali yanayotokea sehemu mbalimbali nchini,” alisema Dk Nagu.
Dk Nagu ambaye alimwakilisha Rais Kikwete katika sherehe hizo, aliliomba kanisa na taasisi nyingine za kidini kuwaandaa waumini wema
ambao watakuwa raia wema.
Alisema dini zote zinahubiri amani, kwa hivyo ni muhimu kuendeleza kwa nguvu jukumu hilo, ili kupunguza uhalifu katika jamii kwa kuwa na raia wema. Kuhusu Uchaguzi Mkuu, Dk Nagu aliliomba
kanisa kuiombea nchi ili ipite kwa amani katika mchakato huo.
Suala la amani ya nchi kwa sasa ni gumzo kubwa kutokana na Taifa kuelekea kwenye Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba, huku kukiwa na viashiria vya amani kuvunjika kutokana na matukio yaliyojitokeza katika uchaguzi wa Serikali za mitaa
uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Akitoa salamu za shukrani baada ya kusimikwa madarakani, Askofu Massangwa aliwataka viongozi wa Serikali na Watanzania wote
kuhakikisha matukio makuu yanayoikabili Taifa mwaka huu ya kura ya maoni ya Katiba mpya na Uchaguzi Mkuu yanafanyika kwa amani na utulivu
na kuliacha Taifa salama.
Katika hafla hiyo, Mchungaji Gideon Kivuyo alisimikwa kuwa Askofu Msaidizi wa Dayosisi hiyo. Nafasi hiyo ilibaki wazi tangu katikati ya mwaka jana kufuatia kifo cha Askofu Thomas
Laizer.
Chapisha Maoni