Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amekiri kuwa
mambo yamekuwa magumu kwa upande wao
katika michuano ya hatua ya makundi ya Kombe la
Shrikisho Afrika na kwamba wanarudi kujipanga
upya kwa ajili ya mwakani.
Yanga ilikubali kipigo cha mabao 3-1 mbele ya
wapinzani wao, Medeama ya Ghana juzi ukiwa ni
mchezo wa nne wa michuano hiyo na kuiacha
timu hiyo ikiendelea kuburuza mkia huku ikiwa
imebakiwa na mechi mbili kabla ya kumalizika kwa
hatua hiyo ya makundi.
Pluijm anasema matokeo hayo yamewapa funzo
kubwa na kama kocha analazimika kukitathmini
upya kikosi chake kabla ya kuelekea kwenye
mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
“Tuliingia uwanjani tukiwa na matumaini makubwa
ya kupata ushindi hasa ukizingatia huo ndiyo
mchezo uliokuwa umebeba matumaini yetu ya
kufika kule tulipopataka, lakini baada ya nusu saa
mambo yakawa tofauti na kubwa ni uzoefu wa
wachezaji wangu hasa wale wa nafasi ya ulinzi
hawakucheza kwa kiwango chao,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alisema ukiacha makosa ya walinzi
wake, kwa ujumla wachezaji wake walicheza chini
ya kiwango na kuwapa nafasi wenyeji wao
Medeama kufanya wanavyotaka na kufunga mabao
hayo ya haraka ambayo alikiri yalichangia kuwatoa
mchezoni.
Alisema kukosekana kwa beki raia wa Togo,
Viccent Bossou nako kulichangia wao kupoteza
mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao kutokana
na uzoefu aliokuwa nao kwenye michuano
mikubwa kama hiyo, lakini atahakikisha wanarudi
kujipanga ili kumalizia mechi zao mbili zilizobaki
ambazo amepania kuhakikisha wanashinda.
Matokeo hayo yamepoteza kabisa matumaini ya
kocha Pluijm kuiona Yanga ikicheza nusu fainali ya
michuano hiyo kwa mwaka huu, baada ya kupata
pointi moja katika michezo minne waliyocheza
huku wakifungwa mechi tatu na kutoka sare
mchezo mmoja na sasa wanahitaji miujiza ili
kufuzu hatua hiyo ya nusu fainali.
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni