SERIKALI imesema muda si mrefu inatarajia kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100, kutokana na washirika wa maendeleo kuanza
kupunguza ufadhili na misaada katika miradi
hiyo.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, wakati akijibu swali
la nyongeza la Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa
(CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali itaacha
kutegemea wafadhili katika kutekeleza miradi ya
maendeleo.
Ngalawa pia alitaka kujua ni lini serikali itajenga
miundombinu ya umwagiliaji nchi nzima ili
kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Lwenge
alisema kwa sasa washirika wa maendeleo
wamepunguza kusaidia miradi ya maendeleo,
jambo ambalo limeifanya serikali kujipanga
kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa
fedha za ndani kwa asilimia 100.
Akijibu swali la pili la nyongeza la Ngalawa, Naibu
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe
alisema zipo hekta milioni 29.4 za kutekeleza
miradi ya umwagiliaji kwa kuziwekea
miundombinu na kwa mwaka huu, hekta milioni
12 zitajengwa miundombinu ya umwagiliaji.
Katika swali la msingi, Ngalawa alitaka kujua
mpango wa serikali wa kuliendeleza bonde la Mto
Ruhuhu lililopo katika kata ya Ruhuhu wilaya ya
Ludewa, ambalo ni eneo muhimu sana na
linaweza kuzalisha mazao mengi na kupunguza
uhaba wa chakula Tanzania.
Kamwelwe alisema Serikali inatambua umuhimu
wa bonde hilo, ambapo katika maandalizi ya
uendelezaji wa bonde hilo upembuzi wa awali
ulifanyika kati ya mwaka 2013 na 2014.
Alisema walibaini uwezekano wa kujenga bwawa
kubwa katika eneo la Kikonge kwa ajili ya
matumizi mbalimbali ikiwemo kudhibiti mafuriko
katika bonde la mto Ruhuhu, kuendesha kilimo
cha umwagiliaji kwa eneo la takribani hekta 4,000
na kufua umeme mkubwa utakaounganishwa
kwenye gridi ya Taifa.
Alisema kwa sasa serikali kwa kushirikiana na
benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ipo katika
hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya
upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa
na miundombinu ya umwagiliaji.
Chapisha Maoni