0

Baada ya kuwa na shida mwanzoni mwa msimu
kupata kikosi cha kwanza na mfumo bora, Antonio
Conte, Meneja wa Chelsea ameweza kufaulu
mtihani huo kwani amefanikiwa kutengeneza kikosi
imara ambacho kina uwezo wa kuleta ushindani na
pengine hata kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya
Uingereza msimu huu.
Nimeanza na maneno hayo baada ya kuishuhudia
Chelsea ikiirarua Manchester United mabao 4-0
katika mchezo wa ligi kuu ya Uingereza uliopigwa
kwenye dimba la Stamford Bridge Jumapili jioni.
Wakitumia mfumo wa 3-4-3, Chelsea walikuwa
hatari toka kupulizwa kipenga cha kuanza
mpambano huo na iliwachukua sekunde 30 tu
kuandika bao la kwanza kupitia kwa Pedro.
Manchester United ikitumia kikosi kilichopata sare
dhidi ya Liverpool Jumatatu iliyopita, ilishindwa
kabisa kufurukuta mbele ya vijana wa Conte
waliokuwa wakiziba kila nafasi.
Cahili, Hazard na Kante walifunga mabao mengine
matatu katika mchezo ambao Chelsea walistahili
kushinda.
Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Jose Mourinho,
Meneja wa Manchester United kurejea Stamford
Bridge akiwa na timu nyingine. Aliondoka na
ushindi mwaka 2010 akiwa na Inter Milan.
Hicho pia ndio kipigo kikubwa zaidi kwa Jose
Mourinho katika miaka yote aliyofundisha soka
nchini Uingereza.
Manchester United walionekana kupooza sana, ni
dhahiri Mourinho bado ana kazi kwani bado hana
timu inayoweza kurudisha enzi za mataji Old
Trafford licha uwekezaji mkubwa uliofanywa kuleta
wachezaji muhimu msimu huu.
Hata hivyo mashabiki wa Chelsea walionyesha
uungwana kwa Mourinho Meneja wao wa zamani
kwa kusimama na kumshangilia baada ya
mwamuzi kumaliza mpambano huo.
Mourinho alikuwa Meneja wa Chelsea kwa vipindi
viwili tofauti huku akiiwezesha timu hiyo kutwaa
mataji matatu ya Premia Ligi.
Jumatano ijayo Manchester United itaumana na
Manchester City kwenye mchezo mwingine
mgumu wa kombe la ligi.



Like Page ya Facebook Africa Newss Sports Posted: ⚽ Africa News Sports2

Chapisha Maoni

 
Top