Washtakiwa 11 wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi wamegoma kushuka kizimbani katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu wakishinikiza kuelezwa jalada la kesi yao lipo wapi na imefikia katika hatua gani.
Sakata hilo lilitokea jana majira ya saa 4:00 asubuhi, muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Peter Njike kumueleza Hakimu Mkazi, Hellen Liwa kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi
wake bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa kutajwa.
Baada ya wakili Njike kueleza hayo, mshtakiwa Longishu Losingo alidai mahakamani hapo kuwa Desemba 16,2014 upande wa mashtaka uliwaambia jalada la kesi yao lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), leo (jana) wanatuletea hadithi, tunaomba watueleze uhalisia wa kesi hii, tupo
gerezani tunateseka.
Kwa upande wa mshtakiwa Masunga Makenza naye alidai kuwa yeye hafahamu sheria, kesi yao ni ya muda mrefu na akahoji jalada likienda kwa
DPP linatakiwa kukaa kwa muda gani.
Makenza alidai kuwa kesi yao ni ya kubambikiwa na kwamba ingekuwa ni kesi halisi upande wa mashtaka ungekuwa umekwisha kamilisha
upelelezi wao na kwamba wao wapo tayari kushtakiwa ila kama upande wa mashtaka umeshindwa kukamilisha upelelezi mahakama iwaachie huru, wakikamilisha watawakamata tena.
Wakili wa Serikali, aliieleza mahakama kuwa wameyasikia malalamiko hayo na kwamba yote yanajikita katika kuchelewa kukamilika kwa upelelezi na kwamba watahimiza na kufuatilia
upelelezi ukamilike mapema.
Jibu hilo halikuwaridhisha washtakiwa hao, mshtakiwa Longishu alisema “Tumechoka kwa kweli tumechoka hatuna ugomvi na mahakama wala magereza ila tunaugomvi na waendesha
mashtaka kama wameshindwa kukamilisha upelelezi watupeleke polisi.”
Yote kwa yote washtakiwa hao, wakaiambia mahakama kuwa kutokana na hoja hizo za upande wa mashtaka leo (jana) hawapo tayari kushuka kizimbani, watakaa chini hadi waelezwe jalada lao lipo wapi na kesi imefikia katika hatua
gani.
Baada ya washtakiwa hao wote kugoma kushuka kizimbani na kukaa chini wakisubiri kuelezwa hatma ya kesi yao, Hakimu Liwa aliwasihi wakubali kuondoka kizimbani hapo kwa sababu
yeye siyo hakimu husika ameitaja tu kesi yao, wamsubiri hakimu husika, Waliarwande Lema wamueleze malalamiko yao.
Maelezo hayo ya hakimu Liwa walikubaliana nayo na kwa pamoja wakainuka na kuelekea mahabusu
ya mahakama kwa ajili ya kupelekwa mahabusu na kesi iliahirisha hadi Januari 13,2015.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Chibago Magozi (32), John Mayunga (56),Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda
Mlewa (40), Zacharia Msese (33), Msungwa Matonya (30), Ahmad Kitabu (30).
Kwa pamoja wanadaiwa kuwa Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa hilo la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho
mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walifanya mauaji hayo katika eneo la Msakuzi Kiswegere lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni ambapo kwa pamoja
walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi ambaye alizikwa kijijini kwake, Chanjale, Kisangara Juu.
Chapisha Maoni